Takwimu zilizotolewa juzi na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika sekondari za Serikali na vyuo vya ualimu mwaka huu zinasononesha na zimethibitisha pasipo kuacha shaka kwamba nchi yetu inaelekea kuzimu katika suala zima la elimu.
Hatuhitaji kupiga ramli kujua kwamba Serikali isipochukua hatua stahiki haraka iwezekanavyo, hata mafanikio kiduchu tuliyokwisha kuyapata yatapotea na kuiacha sekta nzima ya elimu ikiwa mfu. Tunasema hivyo kutokana na takwimu za kutisha zilizotangazwa na wizara hiyo juzi kuonyesha kwamba kutakuwa na upungufu wa wanafunzi 10,074 wa kidato cha tano katika sekondari zinazomilikiwa na Serikali.
Picha halisi ni mbaya zaidi kulikoile iliyoonyeshwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Philipo Mulugo wakati alipotangaza uteuzi wa wanafunzi hao katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi. Jambo ambalo hakulitaja pengine kwa makusudi au kwa bahati mbaya ni ukweli kwamba upungufu wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu utakuwa mkubwa zaidi kwa kuwa zaidi ya robo ya wanafunzi waliochaguliwa kuingia katika sekondari na vyuo vya Serikali watajiunga na sekondari za watu binafsi. Hivyo, hapa tunazungumzia upungufu wa wanafunzi wapatao 13,000 hivi.
Kwa hiyo, tunaishauri Serikali ilione tatizo hilo katika mapana yake, kwa maana ya kuliona kama janga la kitaifa na kulifanya kipaumbele cha kwanza katika mipango ya maendeleo. Elimu ni suala mtambuka kwa sababu inagusa kila sekta, zikiwamo nishati, maji, miundombinu na kilimo ambazo zimetajwa kuwa vipaumbele vya Serikali katika mwaka huu wa fedha. Ndiyo maana tunasema fedha zinazotengwa kila mwaka kwa ajili ya elimu zisipungue asilimia 30 ya bajeti ya Serikali na hili linawezekana iwapo tu tutapunguza vipaumbele ili mkazo uwekwe kwenye elimu.
Lazima tufike mahali tukiri kwamba moja ya changamoto kubwa zinazotukabili kama taifa ni kushuka kwa viwango vya elimu kwa kasi ya kutisha. Takwimu zilizotolewa na Serikali juzi kuhusu ufaulu wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ualimu hazitoi taswira nzuri ya mfumo wetu wa elimu, kwani vigezo vya kujiunga na taasisi hizo viko chini mno, ingawa nafasi nyingi hazikujazwa kutokana na wanafunzi wengi kushindwa hata kufikia vigezo hivyo vya chini.
Ni maeneo gani tumeendelea kufanya makosa? Tumeendelea kupeleka katika vyuo vya ualimu wanafunzi ambao hawakufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne. Nchi zinazothamini elimu hupeleka katika vyuo vya elimu wanafunzi waliofanya vyema katika mitihani ya sekondari, hasa ya kidato cha sita. Sisi tumeendelea kufanya makosa kwa kupeleka wanafunzi walioshindwa kidato cha nne kusomea ualimu, kwani hawawezi kujenga misingi mizuri kwa watoto na badala yake wanaporomosha viwango vya elimu.
Kwa jumla, kutokuwapo wanafunzi wa kutosha kujaza nafasi za kidato cha tano katika sekondari 207 za Serikali pamoja na kupeleka walioshindwa kidato cha nne kusomea ualimu ni hali itakayosababisha janga kubwa kwa nchi yetu katika siku za usoni. Sasa tutazamie vyuo vikuu kukosa wanafunzi na vile vya binafsi kufungwa, huku tukibaki nyuma kielimu tofauti na wenzetu. Hayo ndiyo matokeo ya kuipa elimu kisogo miaka nenda miaka rudi.
No comments:
Post a Comment